Katika hatua nyingine muhimu, kikao cha Ushirika wa Mradi wa Pamoja wa Korosho (KCJE Ltd) pia kiliambatana na zoezi la ugawaji wa vyeti kwa Vyama Wanachama vilivyokidhi masharti ya uanachama kwa mujibu wa katiba na miongozo ya ushirika.

Vyeti hivyo vilitolewa kwa vyama vilivyofanikiwa kulipa ada ya kiingilio pamoja na kukamilisha ununuzi wa hisa zote, jambo linaloonesha uwajibikaji, utii wa taratibu na dhamira ya dhati ya kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya ushirika.
Vyama vilivyopokea vyeti ni:
TAMCU

Lindi Mwambao

RUNALI

TANECU

Uongozi wa KCJE Ltd ulivipongeza vyama hivyo kwa kuonesha mfano bora wa utekelezaji wa wajibu wao wa kisheria na kiushirika, huku ukisisitiza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kuimarisha misingi ya ushirika imara na endelevu.
Hata hivyo, vyama CORECU na MAMCU havikupata vyeti katika awamu hii kutokana na kutokukamilisha masharti ya Uanachama, ikiwemo kulipa ada husika na kununua hisa stahiki. Uongozi wa ushirika ulivitaka vyama hivyo kuchukua hatua za haraka ili kukamilisha taratibu hizo, ili navyo vipate haki na fursa sawa kama wanachama wengine.
KCJE Ltd inaendelea kusisitiza kuwa uwajibikaji wa kifedha na utii wa kanuni ni nguzo muhimu katika kujenga ushirika wenye nguvu, unaolenga kuleta manufaa ya kweli kwa wakulima wa korosho na jamii kwa ujumla.




