Ushirika wa Mradi wa Pamoja wa Korosho (KCJE Ltd) umefanya kikao chake cha kwanza cha robo ya mwaka 2025/2026 kwa mafanikio makubwa, kikao ambacho kilifanyika katika Ukumbi wa Eden Hotel, Mtwara. Kikao hicho kimewakutanisha wajumbe wake wakuu ambao ni Wenyeviti wa Vyama Wanachama (Vyama Vikuu) vinavyounda ushirika huu muhimu wa sekta ya korosho.

Lengo kuu la kikao hicho lilikuwa ni kupitia na kujadili agenda mbalimbali za maendeleo ya ushirika, ikiwa ni pamoja na tathmini ya utekelezaji wa shughuli za awali, mipango ya baadaye, pamoja na changamoto zinazoukabili Mradi kwa ujumla. Katika mjadala huo, wajumbe walipata nafasi ya kutoa maoni, mapendekezo na msimamo wa vyama wanachama kwa masuala nyeti yanayohusu ustawi wa Mradi.

Miongoni mwa masuala yaliyojadiliwa kwa kina ni suala la madeni ya mabomba na magunia, ambalo lilijadiliwa kwa msisitizo mkubwa. Wajumbe walikubaliana kuwa madeni hayo yamekuwa kikwazo katika ufanisi wa utekelezaji wa shughuli za Mradi. Katika mjadala huo, wajumbe walihamasishana kwa pamoja juu ya umuhimu wa Vyama Wanachama kulipa madeni yao kwa wakati, wakisisitiza kuwa wao wenyewe ni viongozi wa Vyama hivyo vinavyodaiwa, hivyo wana wajibu wa kuonyesha mfano bora wa uongozi na uwajibikaji.

Aidha, kikao hicho kilishuhudia tukio muhimu la kiutawala ambapo Bw. Mohamed Nassoro Mwinguku, aliyekuwa Kaimu Meneja Mkuu, alipitishwa rasmi na wajumbe kuwa Meneja Mkuu wa Ushirika wa Mradi wa Pamoja wa Korosho (KCJE Ltd). Uamuzi huo ulifikiwa baada ya wajumbe kuridhishwa na utendaji wake, uadilifu pamoja na mchango wake katika kuimarisha uendeshaji wa shughuli za ushirika.


Vilevile, kikao hicho kilihudhuriwa na Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika – Mkoa wa Mtwara, ambaye alitoa maelekezo na ushauri muhimu kwa wajumbe. Katika hotuba yake, alikumbusha juu ya umuhimu wa Vyama Wanachama kuwajibika kikamilifu, hususan katika kulipa madeni yao kwa wakati, ili kuhakikisha ushirika unaendelea kuwa imara, endelevu na wenye manufaa kwa wanachama wote.

Kwa ujumla, kikao hicho cha kwanza cha robo ya mwaka kimeacha alama chanya, kikiwa ni chachu ya kuimarisha mshikamano, uwajibikaji na maendeleo ya Ushirika wa Mradi wa Pamoja wa Korosho (KCJE Ltd), huku wajumbe wakionesha dhamira ya dhati ya kulinda maslahi ya wakulima na kuendeleza sekta ya korosho nchini.










