Korosho Cooperative Joint Enterprise (KCJE) Ltd imepata fursa ya kushiriki katika Mkutano wa 12 wa Kamati ya Kiufundi ya Mkutano wa Mawaziri wa Ushirika Barani Afrika (The 12th Technical Committee of the Africa Ministerial Cooperative Conference – TCAMCCO), uliofanyika kuanzia tarehe 9 hadi 11 Juni 2026 katika Hoteli ya Radisson Blu Hotel & Residence, Maputo, Msumbiji.

Mkutano huo wa kimataifa umeandaliwa na International Cooperative Alliance Africa (ICA Africa) na umewakutanisha viongozi wa serikali, viongozi wa vyama vya ushirika, watunga sera, wataalamu wa maendeleo ya ushirika pamoja na wadau mbalimbali kutoka nchi za Afrika kwa lengo la kujadili maendeleo ya sekta ya ushirika, biashara ya kikanda, mifumo ya sheria na sera zinazohusu ushirika.

Kauli mbiu ya mwaka 2026 ilikuwa:
“Empowering Cooperatives for Sustainable Trade and Supply Chains in Africa”
(Kuwezesha Vyama vya Ushirika kwa Biashara Endelevu na Mifumo Imara ya Minyororo ya Ugavi Barani Afrika).
Miongoni mwa maeneo muhimu yaliyojadiliwa ni pamoja na namna vyama vya ushirika vinavyoweza kunufaika na fursa zinazotokana na Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA), kuimarisha mifumo ya kidijitali katika ushirika, kuboresha mazingira ya kisheria na sera, pamoja na kuoanisha maendeleo ya ushirika na Dira ya Afrika ya 2063 (Agenda 2063).

Ushiriki wa KCJE katika mkutano huu umeiwezesha taasisi kupata uzoefu, maarifa na mitandao ya ushirikiano wa kikanda na kimataifa ambayo itachangia kuimarisha shughuli za ushirika wa korosho, kuongeza ushindani wa bidhaa za korosho katika masoko ya Afrika na duniani, pamoja na kuendeleza maendeleo endelevu kwa wanachama na wadau wake.
KCJE inaendelea kujitolea kuimarisha sekta ya ushirika na biashara ya korosho kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ndani na nje ya Tanzania ili kuhakikisha manufaa ya kiuchumi yanawafikia wakulima na wanachama wake kwa ujumla.
KCJE Ltd – Pamoja, Tujenge Uchumi.










