Wadau wa zao la Korosho nchini wametakiwa kuongeza kasi ya uzalishaji na kuimarisha ubora wa zao hilo ili kuiwezesha Tanzania kuwa mzalishaji namba moja wa Korosho barani Afrika.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Adam Kigoma Malima, aliyemwakilisha Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo (Mb), wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Wadau wa Tasnia ya Korosho nchini uliofanyika katika Hoteli ya Morena, mkoani Morogoro.
Mhe. Malima amesema Tanzania ina fursa kubwa ya kuongoza uzalishaji wa Korosho barani Afrika, hivyo wadau wanapaswa kutumia mkutano huo kujadili kwa kina mikakati ya kuongeza tija na kuleta mabadiliko chanya katika tasnia hiyo.
“Tutumie mkutano huu kujadili kwa kina namna ya kuongeza tija na mabadiliko chanya katika zao la Korosho, Tanzania ina nafasi kubwa ya kuwa mzalishaji namba moja barani Afrika,” amesisitiza.

Amesema Serikali imelenga kuongeza uzalishaji wa Korosho hadi kufikia tani milioni moja ifikapo mwaka 2030, akibainisha kuwa ili kufikia lengo hilo, juhudi zaidi zinahitajika katika kuimarisha uzalishaji kwenye mikoa inayolima zao hilo.
Mikoa hiyo ni pamoja na Mtwara, Lindi, Ruvuma, Pwani, Singida, Tanga, Morogoro, Mbeya, Kigoma na Dodoma, pamoja na maeneo mengine yenye uwezo wa uzalishaji wa Korosho.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania, Francis Alfred, amesema mwelekeo wa Serikali si kuongeza ukubwa wa maeneo yanayolimwa Korosho pekee, bali kuongeza tija kwa kila eneo la uzalishaji.
Amesema matumizi ya mbegu bora zinazoweza kustahimili visumbufu, magonjwa na mabadiliko ya hali ya hewa ni muhimu katika kuongeza uzalishaji, huku akisisitiza umuhimu wa tafiti zinazofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) katika kupata teknolojia na mbegu bora za Korosho.
Katika mkutano huo, wadau wameendelea kusisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali, wakulima, vyama vya ushirika, watafiti na sekta binafsi katika kukabiliana na changamoto zinazoikabili tasnia ya Korosho. Ushirikiano huo unalenga kuhakikisha huduma za ugani, pembejeo bora, teknolojia za kisasa za uzalishaji na masoko ya uhakika zinawafikia wakulima kwa wakati.
Aidha, mkutano huo umeweka msisitizo katika kuongeza thamani ya zao la Korosho nchini kupitia uwekezaji katika viwanda vya ubanguaji na usindikaji. Hatua hiyo inatarajiwa kuongeza ajira, kuongeza kipato kwa wakulima na kukuza mchango wa zao hilo katika uchumi wa taifa.

Wadau wameeleza kuwa kuongeza uzalishaji sambamba na kuimarisha usindikaji wa Korosho nchini kutaiwezesha Tanzania kunufaika zaidi na mnyororo mzima wa thamani wa zao hilo, badala ya kutegemea zaidi mauzo ya Korosho ghafi.
Mkutano huo umewakutanisha wadau mbalimbali wa tasnia ya Korosho, wakiwemo Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo anayesimamia Maendeleo ya Mazao na Usalama wa Chakula, Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wabunge kutoka maeneo yanayozalisha Korosho, wakulima pamoja na wadau wengine katika mnyororo wa thamani wa zao hilo.
























