NAIBU WAZIRI WA KILIMO ATEMBELEA BANDA LA KCJE NGONGO LINDI

whatsapp image 2026 08 06 at 8.20.19 am


Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. David Silinde, alitembelea banda la Korosho Cooperative Joint Enterprise (KCJE) Limited katika Maonesho ya Nanenane Kanda ya Kusini yaliyofanyika katika Viwanja vya Ngongo, mkoani Lindi.

Ziara hiyo ililenga kujionea huduma na teknolojia mbalimbali zinazotolewa na KCJE katika kuimarisha sekta ya Korosho na maendeleo ya Ushirika nchini.


Akiwa katika banda hilo, Mhe. Silinde alipata maelezo kuhusu shughuli za KCJE, ikiwemo uratibu wa upatikanaji wa pembejeo, huduma kwa wakulima na juhudi za kuongeza thamani ya zao la Korosho kupitia mfumo wa Ushirika.


Katika ziara hiyo, Afisa TEHAMA wa KCJE Maneno Kapuli, alimueleza Naibu Waziri namna KCJE inavyoshirikiana na Vyama vya Ushirika na wadau mbalimbali kuhakikisha wakulima wanapata huduma na pembejeo kwa wakati, pamoja na kuweka mazingira yanayowawezesha kuongeza tija katika uzalishaji wa korosho.


Kadhalika alielezwa hatua zinazochukuliwa katika kuwawezesha wakulima na Vyama vya Ushirika kupata huduma zinazolenga kuboresha uzalishaji, utunzaji wa mazao na upatikanaji wa masoko, sambamba na kuhamasisha uchakataji na uongezaji thamani wa korosho.

whatsapp image 2026 08 06 at 8.20.20 am
Naibu Waziri wa Kilimo David Silinde akisalimiana na watu mbalimbali nje ya banda la KCJE


Ziara ya Naibu Waziri katika maonesho hayo, imeonyesha umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali, Vyama vya Ushirika na wadau wa sekta binafsi katika kuendeleza zao la korosho na kuongeza mchango wake katika uchumi wa wakulima na Taifa.


Maonesho ya Nanenane Kanda ya Kusini katika Viwanja vya Ngongo, Lindi, yanatoa fursa kwa wananchi, wakulima, wafanyabiashara na wadau mbalimbali kujifunza kuhusu teknolojia, huduma na fursa zilizopo katika sekta ya kilimo na Ushirika.

Related Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *