Kaimu Meneja Mkuu wa Korosho Cooperative Joint Enterprise (KCJE) Limited, Spicener Rugalela, amesema taasisi hiyo imepokea shehena ya tani 5,500 za salfa ya unga katika Bandari ya Mtwara kwa ajili ya kuendelea kusambaza kwa wakulima wa korosho katika msimu wa 2026/2027.
Rugalela amesema KCJE imelenga kusambaza jumla ya tani 35,000 za salfa kwa wakulima katika msimu huo, ambapo hadi sasa tani 18,704 tayari zimesambazwa.
Amesema pamoja na shehena hiyo iliyowasili Mtwara, tani nyingine 2,900 zilipokelewa katika Bandari ya Dar es Salaam na zitasafirishwa kwenda mkoani Mtwara kwa ajili ya kusambazwa kwa wakulima.
“Tunapokea tani 5,500 Mtwara na tani nyingine 2,900 zinapokelewa Dar es Salaam, shehena hizo zitasaidia kuendelea na usambazaji wa salfa kwa wakulima wenye mahitaji,” amesema Rugalela.

Amesema kukamilika kwa usambazaji wa shehena hizo kutaifanya KCJE kufikisha tani 27,104, sawa na takribani asilimia 77 ya lengo la tani 35,000 kwa msimu wa 2026/2027.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), Francis Alfred, amesema hali ya zao la korosho mashambani kwa sasa ni nzuri, huku tathmini ikiendelea kubaini maeneo ambayo bado yana mahitaji ya salfa.
Amesema tathmini hiyo inalenga kuhakikisha salfa inawafikia wakulima wenye mahitaji na hivyo kusaidia kuongeza tija katika uzalishaji wa korosho.

Aidha Francis, ameiponeza KCJE kwa kufanya vizuri katika kutekeleza jukumu la kuhakikisha pembejeo zinapatikana na kusambazwa kwa wakulima.
Amesema hatua hiyo ina mchango katika maandalizi ya msimu wa korosho 2026/2027, ikiwemo kuwawezesha wakulima kupata pembejeo wanazohitaji kwa ajili ya kuongeza tija katika uzalishaji.
