Mradi wa Pamoja wa Vyama Vikuu vya Ushirika vinavyolima zao la Pamba nchini (TANCCOOPS), ulifanya ziara mkoani Mtwara kwa lengo la kuitembelea Korosho Cooperative Joint Enterprise (KCJE) Limited ili kujifunza kuhusu shughuli, mifumo na uzoefu wa taasisi hiyo katika kuendeleza sekta ya kilimo.
Ziara hiyo ya siku tatu ilianza Agosti 18, 2026 mkoani Mtwara, ikiwa na lengo la kuupa ujumbe huo fursa ya kufahamu kwa kina namna KCJE inavyotekeleza majukumu yake, hususan katika maeneo ya ushirika, uzalishaji, upatikanaji na usambazaji wa pembejeo pamoja na utoaji wa huduma kwa wakulima.
Katika ziara hiyo, ujumbe wa TANCCOOPS ulianza kwa kutembelea pia Ofisi ya Mrajis Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Mtwara pamoja na Ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Mtwara.

Akizungumza wakati wa kuupokea ujumbe huo, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mtwara, Robert Misungwi, amepongeza hatua hiyo, akisisitiza umuhimu wa taasisi na Vyama vya Ushirika kubadilishana uzoefu na kujifunza mifumo inayoweza kuimarisha ushirika na kuongeza tija kwa wakulima.
Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa KCJE, Mohamed Mwinguku, ameeleza shughuli zinazotekelezwa na taasisi hiyo pamoja na mafanikio yaliyopatikana katika kuwaunganisha wadau na vyama vya Ushirika katika kuendeleza sekta ya kilimo.
Mwinguku amesema KCJE imefarijika kupokea ujumbe kutoka TANCCOOPS katika ziara hiyo yenye lengo la kujifunza na kubadilishana uzoefu kuhusu shughuli za ushirika, hususan katika usimamizi na usambazaji wa pembejeo kwa wakulima.
“Tumefarijika kupokea ugeni kutoka TANCCOOPS, Tunaamini ziara hii itakuwa chachu ya kubadilishana uzoefu, kujifunza na kuimarisha ushirikiano katika kuwawezesha wakulima kupata huduma na pembejeo kwa wakati,” amesema Mwinguku.

Amesema ziara hiyo ni fursa muhimu kwa taasisi hizo kujifunza kutokana na uzoefu wa kila upande, kuimarisha ushirikiano na kubuni mbinu bora zitakazosaidia kuboresha huduma kwa Vyama vya Ushirika na wakulima nchini.
Aidha, Mwinguku amesema KCJE inaendelea kuthamini ushirikiano na wadau mbalimbali wa sekta ya ushirika na kilimo, akieleza kuwa ushirikiano huo ni muhimu katika kuboresha mifumo ya huduma kwa wakulima, kuongeza tija na kuimarisha maendeleo ya vyama vya ushirika nchini.
Katika ziara hiyo, ujumbe huo ulitembelea maeneo mbalimbali ya shughuli za KCJE, ikiwemo maghala, ambako ulijionea namna uhifadhi na usimamizi wa pembejeo unavyofanyika.

Ziara hiyo ililenga kuipa TANCCOOPS fursa ya kujifunza uzoefu wa KCJE katika utekelezaji wa shughuli zake, hususan katika kuhakikisha wakulima wanapata pembejeo na huduma muhimu kwa wakati.
TANCCOOPS inaundwa na Vyama Vikuu vya Ushirika 13 vya zao la pamba kutoka mikoa mbalimbali nchini, ikiwemo Tabora, Shinyanga, Simiyu, Singida, Mara, Mwanza na Geita, miongoni mwa mikoa mingine.










