Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Abdallah Mwaipaya, ameipongeza Korosho Cooperative Joint Enterprise (KCJE) Limited kwa mafanikio makubwa iliyoyapata katika kuimarisha sekta ya korosho nchini, akisema taasisi hiyo imekuwa nguzo muhimu ya kuinua uchumi wa wakulima na kuimarisha Ushirika.
Akizungumza wakati wa kufungua Mkutano Mkuu wa Tano wa KCJE Limited, uliofanyika Julai 15, 2026 mkoani Mtwara, Mwaipaya alisema taasisi hiyo imeonyesha mafanikio ya kipekee katika kuratibu huduma muhimu kwa wakulima, hatua inayochochea ongezeko la tija na ubora wa zao la korosho.
“KCJE imekuwa mfano wa kuigwa katika Ushirika, Mafanikio mliyoyapata yanaonesha wazi kuwa mna uongozi imara, mshikamano na maono ya pamoja ya kuwaletea wakulima maendeleo,” alisema.
Alitaja baadhi ya mafanikio hayo kuwa ni pamoja na kuimarika kwa upatikanaji wa pembejeo za kilimo, vifaa vya kufungashia mazao, mizani ya kidijitali na viuatilifu, huduma ambazo zimewasaidia wakulima kuongeza uzalishaji na ubora wa korosho zao.
Mwaipaya alisema hatua ya KCJE kuimarisha mifumo ya usimamizi wa fedha na utawala bora imeongeza imani ya Serikali, wanachama na wadau mbalimbali, na kuifanya taasisi hiyo kuwa miongoni mwa Vyama vya Ushirika vinavyoaminika zaidi nchini.

Wajumbe wa Bodi ya KCJE wakifuatilia kwa makini hotuba ya mgeni rasmi.
Alisema mafanikio hayo yanakwenda sambamba na juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambayo imeendelea kuboresha mazingira ya sekta ya Korosho kupitia sera rafiki na uwekezaji katika mnyororo wa thamani.
Aidha, aliipongeza KCJE kwa kuendelea kubuni mbinu mpya za kuongeza mapato, kuwekeza katika teknolojia na kuimarisha ushirikiano na taasisi za kifedha pamoja na wadau wa maendeleo, hatua alizosema zinaiweka taasisi hiyo katika nafasi nzuri ya ushindani.
Hata hivyo, aliwataka viongozi wa KCJE kuendeleza mafanikio hayo kwa kuzingatia uwajibikaji, uwazi na uadilifu katika usimamizi wa rasilimali, akisisitiza kuwa uaminifu ndio msingi wa mafanikio ya taasisi yoyote ya Ushirika.
“Endeleeni kulinda imani ya wakulima na Serikali kwa kuhakikisha kila hatua mnayochukua inaleta tija na maendeleo ya kweli kwa wanachama wenu,” alisisitiza.
Akihitimisha, Mwaipaya aliwapongeza Mwenyekiti wa Bodi, menejimenti na wanachama wa KCJE kwa kujenga taasisi imara na yenye mafanikio, akisema Serikali itaendelea kushirikiana nao ili kuifanya sekta ya korosho kuwa chachu ya maendeleo ya Taifa.
