Korosho Cooperative Joint Enterprise (KCJE) Limited imeendelea kupongezwa kwa juhudi zake za kuwajengea uwezo wadau wa sekta ya Ushirika, kupitia mafunzo yanayolenga kuongeza uelewa kuhusu shughuli, majukumu na huduma zinazotolewa na taasisi hiyo.
Pongezi hizo zimetolewa na Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Mtwara, Robert Nsunza, wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya wadau wa KCJE yaliyofanyika Julai 14, 2026 katika Hoteli ya Tiffany mkoani Mtwara.
Nsunza alisema ushirikishwaji wa wadau ni nguzo muhimu ya maendeleo ya Ushirika, akieleza kuwa moja ya misingi ya Ushirika inasisitiza ushirikiano baina ya Vyama vya Ushirika na wadau mbalimbali.
Aliongeza kuwa hata Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC), imeweka kipaumbele katika kuimarisha ushirikiano huo kwa kuwa maendeleo ya sekta hayawezi kufikiwa bila vyama vya Ushirika kushirikiana kwa karibu na wadau wake.
“Mafunzo haya ni hatua muhimu katika kujenga Ushirika imara, wadau wakielewa majukumu ya KCJE watakuwa sehemu ya mafanikio yake na maendeleo ya sekta ya Ushirika kwa ujumla,” alisema Nsunza.

Akizungumza katika mafunzo hayo, Meneja Mkuu wa KCJE, Mohamed Mwinguku, alisema taasisi hiyo itaendelea kutoa mafunzo na elimu kwa wadau wake ili kuwajengea uwezo wa kutumia kikamilifu fursa zinazopatikana kupitia shughuli za Ushirika.
Mwinguku alisema elimu hiyo ni sehemu ya mkakati wa KCJE wa kuhakikisha wadau wanakuwa na uelewa wa kutosha kuhusu huduma zinazotolewa na taasisi hiyo na namna zinavyoweza kuchangia kukuza uzalishaji wa mazao ya Korosho, Ufuta na Mbaazi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa KCJE, Odas Mpunga, alisema tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo mwaka 2022, imepata mafanikio makubwa yaliyosaidia kuimarisha sekta ya Ushirika na kuongeza tija kwa wakulima.
Alitaja mafanikio hayo kuwa ni pamoja na kuboresha upatikanaji na usambazaji wa pembejeo za kilimo, hatua iliyochangia kuongezeka kwa uzalishaji wa korosho katika maeneo mbalimbali nchini.
Aidha, alisema KCJE imeendelea kuimarisha huduma za usafirishaji kwa kununua malori 10 ya kubeba mizigo, hatua inayolenga kuongeza ufanisi wa huduma kwa vyama wanachama na kupunguza gharama za uendeshaji.
“Mafanikio haya yametokana na mshikamano wa Vyama Vikuu vinavyounda KCJE. Tutaendelea kuimarisha huduma zetu ili kuongeza thamani ya mazao na kuinua ustawi wa wakulima,” alisema Mpunga.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mtwara Mwl. Saidi Nyengedi, amepongeza KCJE kwa kuandaa mafunzo hayo, akisema yanaonesha dhamira ya taasisi hiyo ya kujenga ushirikiano na kuwapa wadau maarifa yatakayosaidia kukuza uchumi wa wakulima na maendeleo ya sekta ya Ushirika.
Nyengedi alisema taasisi zinazowekeza katika elimu na kujenga uwezo wa wadau wake huweka msingi imara wa uwajibikaji, uwazi na maendeleo endelevu, huku akiwahimiza viongozi wa vyama vya Ushirika kutumia elimu hiyo kuongeza tija katika maeneo yao.
“Elimu ndiyo msingi wa maendeleo, KCJE imeonesha mfano mzuri kwa kuwajengea uwezo wadau wake, na hili litasaidia kuimarisha Ushirika na kuongeza thamani ya mazao ya wakulima wetu,” alisema Nyengedi
Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Pwani Mwinshehe Mlao ameiomba KCJE kuendelea kutoa mafunzo hayo kwa watendaji wengine wa chama hicho kwa ngazi tofauti ili wakawe mabalozi wazuri wa kuyasemea majukumu ya taaisi hiyo kwa wananchi.
“Kabla ya kuwepo hapa sikujuwa kwamba kuna taasisi kama hii ya KCJE ambayo inafanya mambo mazuri kwa ajili ya wakulima na Taifa letu, nawaomba mafunzo kama haya yakatolewe kwa viongozi wetu wa chama, kwa ngazi tofauti ili wananchi wajuwe kazi kubwa mnayofanya katika maeneo yetu” alisema Mlao
Wadau mbalimbali wakiwemo maafisa kilimo, warajisi wasaidizi, taasisi za fedha, na viongozi wa Vyama vya Ushirika na Siasa walipata nafasi ya kushiriki mafunzo hayo ambayo mada mbalimbali ziliwasilishwa.
















Baadhi ya wadau wa Ushirika kutoka mikoa mbalimbali wakifuatilia mawasilisho wakati wa mafunzo yaliyoandaliwa na Korosho Cooperative Joint Enterprise (KCJE) Limited, katika ukumbi wa Tiffany Hoteli mkoani Mtwara.
