Ushirikiano wa Vyama Vikuu vya Ushirika vinavyounda Korosho Cooperative Joint Enterprise (KCJE) Limited umeendelea kuimarisha sekta ya korosho nchini, huku hatua mbalimbali zilizochukuliwa katika usambazaji wa pembejeo zikichangia kuongezeka kwa uzalishaji wa zao hilo na kuboresha huduma kwa wakulima.
Hayo yameelezwa na Meneja Mkuu wa KCJE, Mohamed Mwinguku, wakati akiwasilisha mada kuhusu shughuli, mafanikio, changamoto na mwelekeo wa taasisi hiyo katika mafunzo yaliyowakutanisha wadau wa Ushirika, akisema lengo ni kuwajengea uelewa ili wawe mabalozi wa maendeleo ya sekta ya korosho nchini.
Mwinguku alisema KCJE ilianzishwa kufuatia hitaji la kuwa na taasisi rasmi ya Ushirika itakayoratibu kwa ufanisi ununuzi wa pamoja wa pembejeo na huduma nyingine muhimu zilizokuwa zikisimamiwa na Kamati ya Ununuzi wa Pamoja.
“KCJE imeanzishwa kuwa chombo rasmi cha kisheria kitakachoratibu shughuli za Ushirika na kuhakikisha wakulima wanapata pembejeo kwa wakati, kwa ubora na kwa gharama nafuu zaidi.” alisema
Alisema kupitia mfumo wa ununuzi wa pamoja, KCJE inaratibu ununuzi na usambazaji wa pembejeo na viuatilifu, vifungashio, mizani za kidijitali pamoja na huduma za usafirishaji wa pembejeo kwenda katika Vyama Vikuu vya Ushirika, hatua inayoongeza ufanisi na kupunguza gharama za uendeshaji.
Mwinguku ameeleza matokeo ya jitihada hizo yameonekana wazi ambapo uzalishaji wa korosho umeongezeka kutoka tani 240,159 msimu wa 2021/2022 hadi tani 618,497 msimu wa 2025/2026, sawa na ongezeko la asilimia 157.5.
Aidha, usambazaji wa salfa umeongezeka kwa asilimia 225.8 kutoka tani 13,562 hadi 44,177 kwa misimu mitano huku dawa za maji zikiongezeka kwa asilimia 43.1 na kufikia lita milioni 2.14.
Kadhalika amebainisha kwamba KCJE imeingia ubia wa kumiliki asilimia 10 ya hisa katika Kampuni ya Wakulima Agro Company Limited inayojenga kiwanda cha kuzalisha salfa ya unga mkoani Mtwara, huku ikiwa tayari imepata eneo la kujenga kiwanda cha kubangua korosho katika eneo la Kongani ya Viwanda – Maranje lililopo Halmashauri ya Mji Nanyamba mkoani Mtwara.

Akizungumzia mwelekeo wa taasisi hiyo, Mwinguku alisema KCJE imejiwekea malengo ya kujenga ofisi ya kisasa, kuanzisha bandari kavu mkoani Mtwara, kuwekeza katika biashara ya korosho na ufuta, kuanza biashara ya usafirishaji kwa kutumia malori 10 na kukamilisha usajili wa salfa na viuatilifu vitakavyoagizwa kutoka nje ya nchi.
“Malengo yetu ni kuifanya KCJE kuwa taasisi imara ya kiuchumi inayotoa mchango mkubwa zaidi kwa wakulima, Vyama vya Ushirika na uchumi wa Taifa kupitia uwekezaji wa kimkakati.” alisema Mwinguku
Hata hivyo, amesema taasisi hiyo inaendelea kukabiliwa na changamoto ya kupanda kwa bei za viuatilifu na vifungashio katika soko la dunia, hususan salfa ya unga, jambo linaloongeza gharama za uzalishaji na usambazaji wa pembejeo kwa wakulima.
Akihitimisha wasilisho lake, Mwinguku aliwataka washiriki wa mafunzo kutumia elimu waliyoipata kuwaelimisha wananchi na wakulima kuhusu umuhimu wa KCJE katika kuendeleza sekta ya korosho, akisisitiza kuwa ushirikiano wa wadau wote ni msingi wa mafanikio endelevu ya zao hilo nchini.
