Jumla ya tani 112,303 za korosho ghafi zimeuzwa kwa thamani ya Sh368.57 bilioni katika minada 10 iliyofanyika ndani ya wiki mbili za mwanzo za msimu wa mauzo wa korosho wa 2026/2027.
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), Francis Alfred, amesema mwenendo wa soko umeendelea kuwa mzuri, huku akivipongeza Vyama Vikuu vya Ushirika kwa juhudi za kuhakikisha wakulima wanalipwa fedha zao kwa wakati.
Alfred amesema bei ya juu iliyofikiwa hadi sasa ni Sh3,430 kwa kilo, huku bei ya chini ikiwa Sh2,970 kwa kilo kwa korosho daraja la kwanza.

Amesema mwenendo huo wa bei unaonesha kuwa soko la korosho limeanza vizuri, hali inayotoa matumaini kwa wakulima kuhusu mapato yao katika msimu huu wa mauzo.
“Tunafurahishwa na mwenendo wa minada katika wiki hizi mbili za mwanzo, tunavipongeza Vyama Vikuu kwa juhudi zinazofanyika kuhakikisha wakulima wanapata malipo yao kwa wakati,” amesema Alfred.
Ameongeza kuwa zaidi ya asilimia 99 ya korosho zilizouzwa katika kipindi hicho zilikuwa daraja la kwanza, jambo linaloonesha juhudi zinazofanywa na wakulima na wadau wengine katika kusimamia ubora wa zao hilo.
Alfred amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuzingatia kanuni bora za uzalishaji, uvunaji, ukaushaji na uhifadhi wa korosho ili kuhakikisha linakidhi viwango vinavyotakiwa sokoni.
Amesema ushirikiano kati ya wakulima, vyama vya ushirika na wadau wengine ni muhimu katika kuendeleza mafanikio ya msimu huu na kuhakikisha zao la korosho linaendelea kuwa chanzo muhimu cha mapato kwa wakulima na taifa kwa ujumla.
