Jumla ya kilo 49,093,143 sawa na tani 49,093.143 za korosho ghafi zenye thamani ya shilingi bilioni 160 zimeuzwa katika minada minne iliyoendeshwa na Vyama Vikuu vya Ushirika vya mikoa ya Lindi na Mtwara, katika wiki ya kwanza ya msimu wa mauzo ya korosho wa mwaka 2026/2027.
Minada hiyo ilianza Oktoba 12 na 13, 2026, kupitia Chama Kikuu cha Ushirika MAMCU, kilichouza jumla ya kilo 11,585,342 sawa na tani 11,585.342, kwa bei ya juu ya Sh3,370 na ya chini ya Sh3,110 kwa kilo.
Oktoba 16, 2026, Chama Kikuu cha Ushirika TANECU kiliendesha mnada wake wa kwanza na kuuza kilo 18,991,115 sawa na tani 18,991.115, kwa bei ya juu ya Sh3,430 na ya chini ya Sh3,250 kwa kilo.
Oktoba 17, 2026, Chama Kikuu cha Ushirika Lindi Mwambao Ltd kiliendesha mnada wake wa kwanza katika AMCOS ya Mtama, na kuuza kilo 7,685,914 sawa na tani 7,685.914, kwa bei ya juu ya Sh3,280 na ya chini ya Sh2,970 kwa kilo.
Oktoba 18, 2026, Chama Kikuu cha Ushirika RUNALI kiliendesha mnada wake wa kwanza na kufanikiwa kuuza kilo 10,830,772 sawa na tani 10,830.772 za korosho ghafi, kwa bei ya juu ya Sh3,430 na bei ya chini Sh3,270.

Akizungumzia mwenendo wa minada hiyo Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), Francis Alfred, amesema mauzo hayo yanaonesha ukubwa wa biashara ya korosho na umuhimu wa kusimamia kikamilifu mfumo wa masoko ili kuhakikisha zao hilo linapata thamani inayostahili.
Alfred amewasisitiza wakulima kuzingatia ubora wa korosho kuanzia hatua za uvunaji, ukaushaji, ukusanyaji hadi uhifadhi ili kuongeza ubora na ushindani wa zao hilo sokoni.
Minada yote inaendeshwa kidijitali kupitia mfumo wa soko la bidhaa hapa nchini (TMX).
