KCJE KUSAMBAZA MAGUNIA MILIONI 9.3 MSIMU WA KOROSHO WA 2026/2027

magunia

Meneja Mkuu wa Korosho Cooperative Joint Enterprise (KCJE) Limited, Mohamed Mwinguku, amesema KCJE imejipanga kuhakikisha hakutakuwa na changamoto ya upatikanaji wa magunia katika msimu wa mauzo na masoko ya korosho wa 2026/2027.

Mwinguku amesema makadirio ya uzalishaji wa korosho kwa msimu huo ni tani 750,000, huku mahitaji ya magunia yakikadiriwa kufikia zaidi ya milioni 9.35.

“Kwa msimu wa  2026/2027 tumejipanga vizuri kuhakikisha changamoto za magunia hazijitokezi. Makadirio ya uzalishaji ni tani 750,000, huku mahitaji ya magunia yakikadiriwa kuwa zaidi ya milioni 9.35,” amesema.

Ameeleza magunia hayo yatasambazwa kwenye vyama vyote sita wanachama, vya TANECU, MAMCU, LINDI MWAMBAO, RUNALI, CORECU na TAMCU.

whatsapp image 2026 10 08 at 3.44.16 am
Pichani ni Meneja Mkuu wa KCJE Mohamed Mwinguku

“Kila chama wanachama kina uhitaji wake wa magunia, na sisi KCJE tumejipanga kuhakikisha tunatimiza mahitaji ya kila mmoja katika msimu, hii itafanya kuondokana na changamoto ambazo zilikuwa zinajitokeza kipindi cha mwanzo”, ameeleza Mwinguku

Amesema hadi sasa, jumla ya magunia milioni 13 yamehifadhiwa katika maghala, hali ambayo inaonyesha kuwa kuna akiba ya kutosha ya kukidhi mahitaji ya msimu huo.

“Hii ina maana kwamba, ukilinganisha na mahitaji ya magunia milioni 9.35, tuna ziada ya zaidi ya magunia milioni 3.5,” amefafanua.

Kwa mujibu wa Mwinguku, uwepo wa akiba hiyo unatarajiwa kusaidia kuzuia changamoto za upatikanaji wa magunia katika maghala, vituo vya usafirishaji na maeneo mengine ya mnyororo wa usambazaji wakati wa msimu wa korosho.

Aidha, amesema mifumo ya mizani ya kidijitali imekamilika na ipo tayari kutumika, huku watendaji pamoja na wadau wengine wanaohusika katika mchakato wa ukusanyaji na uuzaji wa korosho wakiwa wamejipanga kuanza kazi.

Mwinguku amesema maandalizi hayo yanalenga kuhakikisha mchakato wa upokeaji, upimaji na usafirishaji wa korosho unafanyika kwa ufanisi katika msimu wa 2026/2027.

Related Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *