Minada ya msimu wa mauzo na masoko ya korosho kwa msimu wa 2026/2027 inatarajia kuanza Oktoba 12, 2026 nchini, badala ya Oktoba 19, 2026 kama ilivyotangazwa hapo awali na Bodi ya Korosho Tanzania (CBT).
Mabadiliko hayo yamekuja baada ya awali kutangazwa kuwa minada hiyo ingeanza Oktoba 19, huku wadau wa sekta ya korosho wakitakiwa kukamilisha maandalizi ya msimu mpya.
Kulingana na taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho nchini Francis Alfred, imesema kurudishwa nyuma kwa tarehe ya kuanza kwa minada kunalenga kutoa fursa kwa wakulima ambao maeneo yao huanza kuvuna korosho mapema.
Hata hivyo amefafanua kuwa, maghala ya vyama vya msingi yanatarajiwa kuanza kupokea korosho kutoka kwa wakulima kuanzia Oktoba 1, 2026, kabla ya kuanza kwa minada hiyo.
Chama Kikuu cha Ushirika cha MAMCU tayari kimetangaza Oktoba 12 kuwa tarehe ya kuanza kwa msimu mpya wa mauzo ya korosho, huku wakulima, vyama vya msingi, wanunuzi na wadau wengine wakitakiwa kukamilisha maandalizi.

Hata hivyo Bodi ya Korosho, imesisitiza umuhimu wa wakulima kuzingatia taratibu bora za uvunaji, ukaushaji na uhifadhi wa korosho ili kulinda ubora wa zao na kuongeza ushindani wake katika masoko.
Aidha, maandalizi yamehusisha mafunzo ya udhibiti wa ubora pamoja na ufuatiliaji wa hali ya maghala yatakayotumika kuhifadhi korosho kabla ya kuuzwa kupitia mfumo wa minada.
Kwa upande wa usafirishaji, Bandari ya Mtwara imeeleza kujiandaa vyema kuhudumia sehemu kubwa ya korosho zinazozalishwa katika ukanda wa kusini.
Taarifa iliyotolewa na Meneja wa Bandari mkoa wa Mtwara Frednand Nyathi, imeeleza kuwa Bandari ya Mtwara inatarajia kushughulikia zaidi ya tani 550,000 za korosho katika msimu wa 2026/2027.
