Viongozi wa Vyama vya Ushirika nchini wametakiwa kuzingatia misingi ya uongozi na utawala bora ili kuongeza uwajibikaji, uwazi na ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wanachama, hatua inayotazamiwa kuchochea maendeleo ya vyama hivyo na kuongeza tija kwa wakulima.
Wito huo umetolewa na Mhadhiri na Mratibu wa Programu wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU) ofisi ya Mkoa wa Lindi na Mtwara, Paulo Anania, wakati akiwasilisha mada ya Uongozi na Utawala Bora kwenye mafunzo ya wadau wa Korosho Cooperative Joint Enterprise (KCJE) Ltd yaliyofanyika Mtwara.
Amesema mafanikio au kushindwa kwa Vyama vya Ushirika hutegemea kwa kiasi kikubwa ubora wa uongozi uliopo, kwani viongozi ndio husimamia utekelezaji wa shughuli na kuunganisha rasilimali watu kuelekea kufikia malengo ya taasisi.
Anania alieleza kuwa uongozi wa kidemokrasia una nafasi kubwa katika kuimarisha ushiriki wa Wanachama kwa kuwashirikisha katika maamuzi, huku pia akifafanua aina nyingine za uongozi zikiwemo wa kiimla, mfumo huria, mlengo wa mabadiliko na mlengo wa kijasiriamali, akisisitiza kuwa viongozi wanapaswa kuchagua mtindo unaojenga ushirikiano, ubunifu na maendeleo ya Chama.

Aidha, aliwataka viongozi kuandaa kizazi kipya cha viongozi kupitia urithishaji wa uongozi, akibainisha kuwa kila mwanachama anapaswa kuonekana kama kiongozi anayesubiri nafasi yake ya kulitumikia Chama.
Aliwakumbusha viongozi kutotumia nafasi zao kujinufaisha kwa jasho la wanachama na wakulima, bali kuunganisha mawazo ya wanachama wote kwa manufaa ya pamoja.
“Kiongozi bora ni yule anayeunganisha mawazo ya watu wengi na kuyaelekeza katika kufikia malengo ya pamoja ya chama, badala ya kujinufaisha binafsi,” alisema Anania.
Kuhusu utawala bora, Anania alisema kila chama kinapaswa kujenga misingi ya ushiriki wa wanachama, uwazi, uwajibikaji, usawa, haki, demokrasia, ufanisi, kuheshimu sheria na kuwa na uongozi wenye maono.
“Utawala bora ndiyo msingi wa mafanikio ya chama, bila uwazi, uwajibikaji na ushiriki wa wanachama, maendeleo ya ushirika hayawezi kupatikana,” alieleza Anania.

Ameonya kuwa changamoto kama usimamizi mbaya wa fedha, ukosefu wa uwazi, ushiriki mdogo wa wanawake na vijana, mawasiliano hafifu na kukosekana kwa mpango wa kuendeleza viongozi vinaweza kudhoofisha Vyama vya Ushirika.
Akihitimisha mafunzo hayo, Anania amesisitiza kuwa utawala bora ndiyo msingi wa mafanikio ya chama chochote cha Ushirika, huku akisisitiza kuwa utawala dhaifu ni sumu inayoweza kudhoofisha maendeleo ya taasisi na kuathiri ustawi wa wanachama wake.
