MWENYEKITI WA CCM MKOA WA MTWARA KCJE IMELETA MABADILIKO MAKUBWA KATIKA SEKTA YA KOROSHO

kthm1162

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mtwara, Mwl. Saidi Nyengedi, ameipongeza Korosho Cooperative Joint Enterprise (KCJE) Limited kwa mafanikio makubwa iliyoyapata katika kipindi cha miaka minne tangu kuanzishwa kwake, akisema taasisi hiyo imekuwa mfano wa utekelezaji wa dhana ya ushirika katika kukuza uchumi wa wakulima wa korosho nchini.

Mwl. Nyengedi alitoa pongezi hizo wakati akizungumza katika Mkutano Mkuu wa 5 wa KCJE Limited, akisema mafanikio ya taasisi hiyo yanadhihirisha utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi inayotambua ushirika kama chombo muhimu cha kuwaletea wananchi maendeleo ya kiuchumi.

Aliwapongeza viongozi wa Vyama Vikuu vya Ushirika vilivyounda KCJE kwa mshikamano wao, akieleza kuwa mafanikio yaliyofikiwa yamejengwa na umoja pamoja na ushirikiano wa wanachama na viongozi wake.

“Kazi iliyofanywa na uongozi na menejimenti ya KCJE ndani ya miaka minne inastahili pongezi. Mmeonyesha kuwa ushirika unaweza kuwa chachu ya maendeleo ya wakulima na uchumi wa Taifa,” alisema.

prxz9668
Wadau mbalimbali walioshiriki katika mkutano mkuu wa tano wa KCJE

Alisema KCJE imefanikiwa kuimarisha upatikanaji wa pembejeo za kilimo, kuratibu huduma kwa wakulima kupitia vyama vya ushirika na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa shughuli zinazolenga kuinua uzalishaji wa korosho.

Kwa mujibu wa Mwl. Nyengedi, mafanikio hayo yameifanya Serikali kuendelea kuiamini KCJE na kuipa majukumu makubwa zaidi katika sekta ya kilimo, ikiwemo kushiriki katika usimamizi wa vituo vya zana za kilimo ili kuboresha huduma kwa wakulima wa mazao mbalimbali.

Aidha, aliipongeza KCJE kwa mikakati yake ya kupanua shughuli zake kwa kuwa na mpango wa kujenga viwanda vya kubangua na kuchakata korosho pamoja na kuongeza thamani ya zao hilo, hatua ambayo alisema itawaongezea wakulima ushindani wa soko na fursa ya kupata bei bora zaidi.

Akizungumzia mafanikio ya sekta hiyo, Mwl. Nyengedi alisema ndani ya miaka minne uzalishaji wa korosho umeongezeka na kufikia zaidi ya tani 600,000, jambo alilosema linaonesha mchango mkubwa wa KCJE katika kuongeza tija na kuinua kipato cha wakulima.

Aliitaka KCJE kuendelea kupanua huduma zake kwa wakulima wa korosho na mazao mengine, kuimarisha ushirikiano na Serikali pamoja na wadau wa sekta ya kilimo ili kuhakikisha ushirika unaendelea kuwa nguzo ya maendeleo ya wakulima na uchumi wa Taifa.

Related Post

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *